10 Aprili 2025 - 19:51
Source: Parstoday
Kuidhinishwa makubaliano ya pande zote baina ya Iran na Russia katika Duma kuna umuhimu gani?

Bunge la Duma la Russia Jumanne (Aprili 8) liliidhinisha Mkataba wa Ushirikiano Kamili wa Kimkakati kati ya Russia na Iran.

Mswada wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Moscow na Tehran uliwasilishwa kwenye Bunge la Duma na Rais wa Russia, Vladimir Putin mnamo Machi 27. Makubaliano haya yalitiwa saini na viongozi wa nchi hizo mbili msimu wa baridi uliopita wakati wa ziara ya Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian huko Moscow.

Kuidhinishwa makubaliano ya pande zote baina ya Iran na Russia katika Duma kuna umuhimu gani?

Rais Pezeshkian na mwenzake wa Russia Vladimir Putin 

Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia unaathiriwa na mambo mengi ya ndani na nje. katika upande wa masuala ya ndani, Iran na Russia ni nchi mbili jirani. Licha ya kuwa kuna mitazamo hasi ndani ya nchi zote mbili kuhusiana na uhusiano wa pande mbili, serikali za nchi mbili daima zimekuwa zikielekea katika kupanua uhusiano.

Mtazamo wa Moscow na Tehran kuhusu utaratibu wa sasa wa mfumo wa kimataifa usio wa haki, pamoja na vitisho vinavyozikabili pande hizi mbili kwa pamoja vya madola ya Magharibi hususan Marekani ni jambo muhimu katika mwelekeo na msisitizo wa Iran na Russia katika kupanua uhusiano wao. Nchi zote mbili zinataka kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na mashinikizo ya Magharibi, hususan vikwazo vya Marekani. Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Moscow na Tehran yanaweza kuonekana kama jibu kwa vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa ya nchi za Magharibi, na yanaonyesha nia ya nchi hizo mbili kuunda kambi mmoja dhidi ya changamoto za pamoja. 

Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Moscow na Tehran pia ni muhimu kwa kuzingatia vipengele vingine kadhaa. Moja ya vipengele muhimu vya mkataba huo ni kwamba unaweza kupelekea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Iran inataka kuvutia uwekezaji na teknolojia ya Russia katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nishati, viwanda na kilimo. Kwa upande mwingine, Russia inaweza pia kufaidiika na maliasili na soko la Iran.

Mbali na umuhimu wake wa kisiasa na kiuchumi, makubaliiano ya kimkakati ya Iran na Russia pia ni muhimu katika masuala ya kijeshi na kiusalama. Makubaliano hayo yanaweza kupelekea kuimarishwa ushirikiano wa kijeshi na kiusalama kati ya Iran na Russia. Ushirikiano huu unaweza kujumuisha kubadilishana taarifa, mafunzo ya kijeshi, na hata uuzaji wa silaha. Wakati nchi zote mbili zinakabiliwa na vitisho vya pamoja kutoka kwa makundi ya kigaidi na vilevile mashinikizo ya kijeshi ya nchi za Magharibi, ushirikiano huu unaweza kusaidia kuongeza usalama wa kitaifa wa nchi hizo.

Kuidhinishwa makubaliano ya pande zote baina ya Iran na Russia katika Duma kuna umuhimu gani?

Rais wa Iran ziarani Russia katika msimu wa baridi uliopita 

Jambo muhimu la kuashiria ni kwamba, licha ya kupitishwa makubaliano katika Duma ya Ruussia na kuandaliwa uwanja wa utekelezaji wake, bado kuna changamoto kubwa katika njia ya kusonga mbele. Moja ya changamoto hizo ni kufanana kwa chumi za nchi hizo mbili. Miundo ya kiuchumi ya nchi hizo mbili haiingiliani sana kwa sababu nchi zote mbili ni wauzaji mafuta nje ya nchi na waagizaji wa teknolojia ya kisasa. Masoko yanayolengwa ya nchi zote mbili ni pamoja na nchi zinazoagiza nishati na malighafi kutoka nje. Kwa sasa  nchi hizi mbili ziko chini ya vikwazo vya Magharibi, na ingawa mbinyo huu umezifanya kuwa karibu zaidi, lakini jambo hili halina maana kukamilishana kiuchumi na kibiashara.

Nukta ya mwisho ni kwamba, licha ya changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Makubaliano ya Kimkakati ya Iran na Russia, lakini kwa upande mmoja, azma ya nchi hizo mbili ya kuimarisha na kupanua uhusiano, na kwa upande mwingine, uanachama wa Tehran na Moscow katika jumuiya na mashirika ya kieneo kama vile Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia na kundi la BRICS, unaweza kuchangia pakubwa katika utekelezaji wa makubaliano hayo.

Your Comment

You are replying to: .
captcha